Wednesday, 25 June 2014

ROZARI YA HURUMA KUU YA MUNGU

 Mtakatifu Maria Faustina

 HISTORIA

Sista Faustina alizaliwa tarehe 25 August 1905 katika kijiji cha Glogowieko nchini Poland, na jina lake la ubatizo lilikuwa Helena.
Akiwa na umri wa kiaka 20, Bwana alimwongoza kuingia katika utawa wa shirika la Mama wa Huruma ambako (kama kawaida) alibadilisha jina na kuitwa Sista Maria Faustina, akaweka nadhiri za kwanza mwaka 1928.

MATUKIO
Bwana Yesu alianza kumtokea Sista Faustina mfululizo tangu mwaka 1930 hadi 1938. Alimtokea ili kumwandaa kwa ujumbe mkubwa wa maisha wa kuitgazia dunia nzima ibada ya Huruma ya Mungu, ambayo ilikuwa na madhumuni yafuatayo;
  1. Kuandaa ujio wa Pili wa Bwana wetu Yesu Kristo aliye Mfalme wa Huruma.
  2. Kuokoa roho zilizoko Toharani.
  3. Kuwaongoa wakosefu ambao wameshapoteza neema ya kujiombea.
  4. Kuitangaza Huruma ya Mungu.
Tarehe 22 Februari 1931 alipokuwa na umri wa miaka 26, Sista Faustina alitokewa kwa mara ya kwanza na Bwana Yesu na kumchagua kuwa mjumbe wa Ibada ya Huruma ya Mungu. Sista Faustina anatueleza:
  


"Jioni, ndani ya chumba changu, huku nikiwa nimepiga magoti kwa woga na furaha, nilimuona Bwana Yesu akiwa amevaa vazi refu jeupe. Aliinua mkono juu kwa kubariki, na mkono mwingine ulishika nguo yake kifuani. Kutoka ndani ya nguo kifuani kulitokea miale ya aina mbili ya mwanga inayong'ara. Miale ya upande wa kulia ilikuwa myekundu na miale ya upande wa kushoto ilikua myeupe" 

YESU NINAKUTUMAINIA

"Mchoro halisi wa Huruma Kuu, uliochorwa chini ya usimamizi wa Sista Faustina"

Sista Faustina hakujua maana ya aina hizo mbili za miale ya mwanga aliyoiona, na siku moja alimuuliza Bwana Yesu maana yake. Bwana Yesu kwa utulivu mkubwa alimwambia, "Miale miwili hiyo ya mwanga inayotoka ndani ya moyo wangu ni alama ya Damu na Maji yaliyomwagika kutoka katika Moyo wangu wenye Huruma, siku ile nilipojitoa sadaka Kalvarini. 
Miale Myeupe ni alama ya Maji yanayoosha roho na miale Myekundu ni alama ya Damu inayoleta uzima wa Roho za watu. Miale hii inalinda Roho kabla ya adhabu ya Baba yangu: Kwa anayeishi katika ulinzi wake (Miale hiyo), mkono wa Hasira ya Mungu hautamfikia kamwe.

Kisha Bwana Yesu alimfundisha Sista Faustina sala hii: "Ee Damu na Maji vinavyotoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, kama chanzo cha Huruma yake, ninakutumaini"

Bwana Yesu huku akimwonyesha Moyo wake Mtakatifu alimwambia Sista Faustina "Chora picha kama unavyoona, na  uandike YESU NINAKUTUMAINIA. Mimi ni Mfalme wa Huruma.
Ninatamani picha hii iwekwe na kuheshimiwa kwanza Kanisani kwako na baadaye Ulimwenguni kote. Naahidi ushindi kwake na maadui zake walio Duniani na hasa saa ya kufa kwake. Mimi mwenyewe nitamlinda. Kwa njia ya picha hii nitatoa neema nyingi kwa watu watakaoitunza vizuri, hata kwa wale watakaoitazama"

AHADI 15 ZA ROZARI TAKATIFU

Mama Bikira Maria alitoa ahadi 15 kwa yule au wale watakaosali Rozari takatifu kila siku. Ahadi hizi aliwapa Mtakatifu Dominic na mwenye heri Alan de la Roche.

1. Yeyote yule atakayesali kwa imani rozari hii takatifu atapokea neema kuu zenye nguvu

2. Naahidi ulinzi wa kipekee na neema za kipekee kwa yule atakayesali rozari hii

3. Rozari itakuwa silaha kubwa dhidi ya nguvu za kuzimu, itaharibu maovu, itapunguza dhambi na kushinda kutofautiana

4. Itafanya fadhila kukua, kazi nzuri kuongezeka, itapatia roho huruma tele toka kwa MUNGU, itaondoa hamu ya wanadamu kupenda mambo ya dunia na majivuno yake na kufanya wapende zaidi mambo ya mbinguni. Ooh, ni kwa namna gani roho hizo zitajifurahisha na kubarikiwa kwa namna hii.

5. Roho zitakazojikabidhi kwangu kwa njia ya kusali rozari, kamwe hazitapotea.

6.  Yeyote atakayesali rozari kwa uaminifu huku akiyatafakari matendo makuu  ya rozari, kamwe hatashindwa na ubaya. MUNGU hatamwadhibu katika hukumu yake, hatapotea katika kifo asichopangiwa na atabaki katika neema za MUNGU na kustahili kupata uzima wa milele.

7. Yeyote atakayekuwa mwaminifu katika kusali rozari, kamwe hatakufa bila ya kupokea Sakramenti takatifu za Kanisa.

8. Wote watakaokuwa waaminifu katika kusali rozari watadumu katika mwanga wa MUNGU katika maisha yao na saa yao ya kufa na kupata neema zake tele; katika saa yao ya kufa watashiriki fadhila za watakatifu waliopo peponi

9. Nitawatoa toharani wale wote waliokuwa waaminifu katika kusali rozari

10. Watoto wangu waaminifu katika kusali rozari watapata fadhila kuu ya utukufu Mbinguni.

11. Utapata yale yote unayoniomba kwa kusali rozari

12. Wote wale wanaoeneza rozari hii takatifu nitawasaidia katika mahitaji yao

13. Nimepata toka kwa mwanangu Mtukufu kuwa mawakili wote wa rozari takatifu watapata
waombezi toka baraza lote kuu la Mbinguni wakati wa maisha yao na wakati wa saa yao ya kufa.

14. Wote wanaosali rozari hii takatifu ni wanangu, na kaka na dada wa mwanangu wa pekee YESU KRISTO

15. Ibada kwa rozari takatifu ni ishara kuu ya kuelekea ukombozi

Saturday, 21 June 2014

MATENDO YA ROZARI

Rozari imegawanyika katika matendo yafuatayo:
Matendo ya FURAHA, UCHUNGU na UTUKUFU.
Na mnamo October 16, 2002 baba mtakatifu marehemu John Paul II aliongeza matendo mengine ambayo yaliitwa matendo ya MWANGA.

MATENDO YA FURAHA (Jumatatu na Jumamosi)

Tendo la kwanza; Malaika Gabrieli anampasha habari Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Tumwombe Mungu  atujalie unyenyekevu.
Tendo la pili; Maria Mtakatifu anakwenda kumtembelea Elizabeti. Tumwombe Mungu atujalie mapendo ya jirani.
Tendo la tatu; Yesu anazaliwa Betlehemu. Tumwombe Mungu atujalie moyo wa ufukara
Tendo la nne; Yesu anatolewa hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie usafi wa moyo.
Tendo la tano; Maria anamkuta Yesu hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie kuwatii wakubwa wetu.

MATENDO YA UCHUNGU (Jumanne na Ijumaa)

Tendo la kwanza; Yesu anatoka jasho la damu kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie sikitiko la dhambi.
Tendo la pili; Yesu anapigwa kwa mijeledi kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuacha dhambi za uchafu.
Tendo la tatu; Yesu anatiwa miiba kichwani kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kushinda kiburi.
Tendo la nne; Yesu anachukua Msalaba kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuvumilia taabu.
Tendo la tano; Yesu anakufa Msalabani. Tumwombe Mungu atujalie kuwapenda Yesu na Maria.

MATENDO YA UTUKUFU (Jumatano na Jumapili)

Tendo la kwanza; Yesu anafufuka. Tumwombe Mungu atujalie kugeuka watakatifu.
Tendo la pili; Yesu anapaa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kwenda mbinguni.
Tendo la tatu; Roho Mtakatifu anawashukia Mitume. Tumwombe Mungu atujalie bidii katika dini yetu.
Tendo la nne; Bikira Maria anapalizwa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kufa vizuri.
Tendo la tano; Bikira Maria anawekwa Malkia mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kudumu katika njia njema.

MATENDO YA MWANGA (Alhamisi)
Tendo la kwanza; Yesu anabatizwa Mto Jordani. Tumwombe Mungu atujalie uaminifu kwa ahadi zetu za ubatizo.
Tendo la pili; Yesu anageuza maji kuwa divai huko Kana. Tumwombe Mungu atujalie kuukoleza ulimwengu kwa chachu ya enjili.
Tendo la tatu; Yesu anatangaza Ufalme wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie kupokea Ufalme wake kwa toba ya kweli.
Tendo la nne; Yesu anageuka sura. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuung’arisha ulimwengu kwa uso wa Yesu.
Tendo la tano; Yesu anaweka Sakramenti ya Ekaristia. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine.

Saturday, 14 June 2014

ROZARI TAKATIFU

Neno Rozari limetokana na neno la Kilatini  "Rosarium" lenye maana ya Taji la Mawaridi.
Mama yetu Bikira Maria aliwafahamisha baadhi ya watu aliowatokea kua kila mara mtu anaposali sala ya "Salamu Maria" anampa mama Maria waridi na hivyo kila anayesali rozari nzima humkabidhi mama Maria taji la mawaridi.

Rozari takatifu hujulikana kama sala kamili kwa sababu ndani yake hupatikana hadithi kamili ya ukombozi wetu sisi wanadamu.
Katika rozari tunatafakari matendo ya Furaha, Uchungu na Utukufu ambayo yanaelezea historia nzima ya maisha ya Bwana wetu YESU KRISTO na ukombozi uliopatikana katika yeye kwetu sisi wanadamu.
Katika sala ya Salamu Maria tunamkaribisha mama Maria atuombee sisi wanadamu kwa mwanawe bwana wetu YESU KRISTO hivyo kufanya sala zetu kuwa na nguvu zaidi mbele zake MUNGU.

YESU hawezi kukataa maombi ya mama yake na hivyo ni wajibu wetu  kufanya bidii katika kusali rozari takatifu ya Mama yetu Bikira Maria.

Dhumuni kuu la kusali rozari ni kwa ajili ya kuwaombea wakosefu waongoke na kumrudia MUNGU katika KRISTO YESU mwanawe wa pekee aliyetukomboa dhidi ya yule muovu kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Kila mara mtu au watu wanapopiga magoti na kusali rozari mama Bikira Maria huja haraka na kukaa pembeni yake/yao wanaosali na kusali nao, na haji peke yake kwa kuwa yeye ni Mama wa MUNGU na Malkia wa Malaika huja na jeshi kubwa la Malaika. Na kwa kuwa yeye ni mama wa YESU, hivyo YESU huja nae pia na YESU ni nafsi ya pili ya MUNGU hivyo MUNGU BABA na MUNGU ROHO MTAKATIFU huja pia kwa sababu hawatengani kamwe.

http://www.theholyrosary.org/